Na
Grace Mwakalinga, Mbeya
“Kutokana na ukata wa fedha kutoka kwa wazazi
wakati mwingine ninalazimika kutumia vitambaa ili kujisitiri, kwa siku
ninatumia vitambaa vitatu mpaka vinne kulingana na hedhi inavyotoka, wakati wa
mapumziko au nikiona nimezidiwa naenda chooni kubadilisha kitambaa kingine,
sijisafishi ninavaa hivyovyo kwa sababu ya tatizo la maji hapa shuleni.”
alisema Nchambi Petro, ambaye ni Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Imezu iliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mkoani Mbeya, katika mahojiano na mwandishi wa
Makala hii.
Petro
ni Dada Mkuu wa Shule, ambaye naye anaishi hosteli anadai ukosefu wa
huduma ya maji kunaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya masomo yao
kwani hutumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji kwenye mifereji na mito
ambaye iko mbali na mazingira ya shule.
Petro
anasema njia pekee ya kutatua changamoto hiyo ni Serikali au wazazi
kukubali kuweka matanki ya kuvuna na kuhifadhi maji katika shule yao wakati wa
Mvua.
Wanafunzi
wa kike katika Shule ya Sekondari Imezu,
iliyopo katika Kata ya Inyala Wilaya Mbeya, wengi wao wanatoka
katika familia za kawaida ambazo pia
kipato cha wazazi ni kidogo. Wengi wanashindwa
kujisitiri na kufanya usafi wa maumbile yao kutokana na changamoto ya ukosefu
wa huduma ya maji safi na salama shuleni hapo.
Wanafunzi
hao wanadai kukosekana huduma ya maji kunachangia kwa kiasi kikubwa watoto wa
kike wanapokuwa kwenye hedhi kutoa harufu mbaya kutokana na kukosa
maji ya kujisafisha.
![]() |
wasichana wa shule za Sekondari wakionesha Pedi ambazo wamepatiwa kama msaada kuwawezesha kuhudhuria masomo vizuri. |
Wanasema
wakati mwingine wakiwa shuleni hulazimika kuficha kiasi kidogo cha maji
ambayo wamechota mtoni kwa ajili kujisafishia ili kukwepa fedheha mbele
za wanafunzi wa kiume.
Tangu
kuanza kwa kidato cha kwanza mwaka 2007, Shule hiyo haijawahi kupata huduma ya
maji safi na salama licha ya kuwa na miundombinu ya mabomba ambayo hayatoi
maji, hali inayowalazimu wanafunzi kuvunja vipindi vya masomo kufuata huduma ya
maji kwenye mito na mifereji.
Licha
ya Shule ya Sekondari Imezu kujenga mabweni kwa ajili ya watoto wa
kike kwa lengo la kuondoa changamoto za mimba kwa wanafunzi wanaotoka
mbali, visa vya ubakaji na kuongeza ufaulu, lakini muitikio wa wazazi au walezi
kupeleka hosteli watoto wao umekuwa mdogo kutokana na changamoto ya maji.
Madhira
ya maji shuleni hapo pia yametajwa na wanafunzi kuongeza utoro kwani wakati
mwingine hulazimika kuondoka shuleni kutafuta maji ya kunywa matokeo yake
wanafunzi kutorudi tena kwenye vipindi vingine vya masomo.
Sharon
Msalilwa ni mwanafunzi wa kidato cha Tatu katika Shule hiyo ambaye anaishi
hosteli anasema changamoto ya maji imekuwa moja ya kikwazo kwa mtoto wa
kike katika kupata elimu kwani awapo kwenye hedhi hukosa amani na morali ya
kusoma.
Anasema
wakati wa kipindi cha hedhi anashindwa kuzingatia masomo kwani muda wote
anajihisi kuwa amechafuka au kuhadhirika mbele ya darasa licha ya kuwa
amejisitiri.
Msalilwa
anaongeza kuwa kukosekana kwa chumba maalum cha kubadilishia taulo za kike ni
changamoto nyingine kwani hutumia vyoo vya kawaida ambavyo alieleza kuwa havina
maji na ni vichafu.
Anasema
kukosekana kwa maji katika vyoo kunaweza kusababisha magonjwa ya U.T.I, kuhara
na hata kipindupindu.
Ruth
Mzinga ni mwalimu na mlezi wa wasichana katika shule ya sekondari
Imezu, anasema ukosefu wa maji shuleni hapo unawaathiri kwa kiasi kikubwa
wanafunzi wa kike kutokana na kuwa maumbile yao kuhitaji zaidi matumizi
ya maji.
Mwalimu
Mzinga anasema ukosefu wa maji shuleni hapo pia umechangia kwa kiasi
kikubwa wazazi au walezi kutowapeleka mabinti wao hosteli.
Mwalimu
Mkuu wa Shule hiyo Tibus Makona amekiri kuwepo kwa changamoto ya ukosefu
wa maji na kueleza kuwa anayeathirika zaidi na kadhia hiyo ni binti.
Anasema
Shule haina uwezo wa kuleta maji licha ya kuwa kuna miundo mbinu ya mabomba
ambayo alisema yanatoa maji mara moja kwa mwezi au wakati mwingine kutotoka
kabisa.
Inasema
idadi kubwa ya wanafunzi shuleni hapo ambayo kwa sasa imefikia wanafunzi
862 wasichana wakiwa ni 488 na wavulana 374 inatoa taswira ya uhitaji mkubwa wa
maji.
Makona
ameleeza kuwa katika kumsaidia mtoto wakati wa hedhi Shule imeweka utaratibu wa
kununua dazani moja ya taulo za kike kwa kila mwezi kwa kutumia fedha ambazo
zimetengwa kwa ajili ya kununulia madawa.
Amesema
taulo hizo za kike hazikidhi mahitaji kwa wanafunzi wote wenye uhitaji lakini
wanamsiadia binti ambaye amepata dharula awapo shuleni.
Hata
hivyo Makona amesema kuwa hosteli inauwezo wa kubeba wanafunzi 160 lakini kwa
sasa ina wanafunzi 34.
Akizungumzia
kadhia ya maji Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ambaye pia ni
Diwani wa Kata ya Inyala, Mwalingo Kisemba, alisema kuwa Serikali
inatambua jinsi changamoto ya maji inavyoathiri elimu ya mtoto wa kike ambapo
amesema kwa sasa wamenunua tanki ambalo litatumika kuvunia na kuhifadhia
maji katika kipindi hiki cha masika.
Licha
ya kuwa Serikali imetoa msaada wa tanki la Maji shuleni hapo ambalo bado
halijatengenezwa miundo mbinu kwa ajili ya kutumika watahakikisha wanafanya
haraka ili kunusuru hali hiyo.
“Mtoto
wa kike hushindwa kuhudhuria masomo siku tano kila mwezi kutokana na sula la
hedhi na miezi miwili kila mwaka, hali hii sio nzuri kwani utoro huo
usababishwa na changamoto ya kukosa taulo za kujisitiri na ukosefu wa maji pia
jitihada zinahitaji ili kuwasaidia mabinti zetu hawa,” alisema Mwalingo.
Naye
Ofisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Mbeya, Zena Kapama alisema kuwa kwa
kutambua changamoto wanazozipata watoto wa kike wawapo shuleni Halmashauri ya
Wilaya ya Mbeya imetenga jumla ya shilingi milioni 1.6 kwa mwaka wa fedha
2018/2019 kwa ajili ya ununuzi wa tatulo za kike ambapo utekelezaji wake
utazinufaisha shule za Sekondari 28 za Wilaya hiyo.
Kapama
anasema wanatambua ukubwa wa tatizo kwa mabinti lakini kwa kuanzia itasaidia na
kuahidi kuongeza bajeti wakati mwingine kadri fedha zitakapopatikana.
TGNP
Mtandao ni taasisi inayojenga uwezo kwa wananchi kuibua suala la upatikanaji wa
pedi za bure kwenye mikutano ya vijiji na mitaa na kuomba serikali za vijiji na
kamati za maendeleo za Kata (WDC) kupanga kwenye bajeti zake ili shule za kata
zitoe bure pedi kwa wasichana.
Hadi
sasa halmashauri tatu ambazo watumishi wake wamejengewa uwezo na TGNP Mtandao
zimeshapanga fedha kwenye bajeti zake
kuwezesha wasichana kupata bure pedi mashuleni. Halmashauri hizo ni Kishapu,
Kisarawe na Mbeya.