Mtandao huu bado upo kwenye matengenezo, punde utapata matukio katika picha, habari, makala na taarifa mbali za kijamii...Endelea kutufuatilia

Monday, May 21, 2018

Ukosefu wa maji safi na salama Kishapu unakwamisha elimu



Na  Kareny  Masasy


Tatizo la maji kwa Kishapu limeendelea kuwa kubwa licha na mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kufikia baadhi ya maeneo. 

WANANCHI  wa kijiji cha Ng’wang’hili  kata ya Bunambiyu  halmashauri ya wilaya ya Kishapu  wamelazimika kuchimba bwawa la maji  kwenye kiwanja cha shule ya msingi ya kijiji hicho ili kuweza kuvuna maji nakuondoa kero ya maji kwa wananchi na wanafunzi wawapo shuleni.

Lakini upatikanaji wa maji hayo umekuwa siyo safi na salama kwani  mazingira  yaliyopo  bwawa hilo siyo salama kwani baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo hasa darasa la awali na la kwanza  hulazimika kujisaidia  nje ya choo cha shule na kinyesi kutapakaa hovyo.

Mwalimu Faustine Kuhenga anasema kuwa bwawa hilo limechimbwa kwa nguvu za wananchi kutokana na uhaba mkubwa wa maji katika shule hii ikiwa hata jamii yenyewe  bwawa hili limekuwa likiwasaidia kwa maji ya  matumizi ya nyumbani na kunywa.
“Bwawa hili lipo katika mazingira ya shule walifanya hivyo ili kuweza kurahisisha huduma ya maji kwa wanafunzi kwaajili ya kunywa  pia jamii yenyewe imekuwa ikilitegemea bwawa kwa kuvuna maji nakuwasaidia kipindi cha kiangazi ingawa hufikia wakati hukauka pia”anasema  mwalimu Kuhenga.

Pia anasema kuwa shule hii ina matundu ya vyoo manne ambayo hutumika lakini baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijisaidia nje ya vyoo   na msimu huu wa mvua  maji hujaa  maeneo yote  nakuchanganyikana lakini bado wanaendelea  kila siku kuwapatia elimu wanafunzi hao kmatumizi ya vyoo.

“Unafahamu  jamii  hapa kijijini bado inamwamko mdogo wa elimu  hata utunzaji wa mazingira kwa maeneo wanayotoka wanafunzi hawa vyoo vyake havina ubora  na umri wao inaonekana wanajisaidia nje ya vyoo hili tumeliona na kila siku kabla ya vipindi hutoa elimu ya  juu ya afya na matumizi ya vyoo lakini bado hawaelewi”anasema mwalimu Kuhenga.
Anasema hata uvunaji wa maji kwenye tanki lililopo husaidia kipindi cha mvua pekee na msimu wa kiangazi hakuna maji na bwawa hili husaidia hadi jamii kwa kipindi kifupi nalo hukauka na kulazimika kwenda kuyafuata maji safi na salama kwenye kijiji cha Ng’wang’osha  umbali wa kilomita  20  kwa baiskeli au wakati mwingine kwa miguu.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho  Shija  Reuben  na  Ester Swilasi wanasema kuwa kuna shida kubwa ya maji kipindi cha kiangazi bwawa la shule  lilichimbwa ili kuvuna maji  kipindi cha masika nakuweza kuwasaidi wanafunzi hata jamii yenyewe nalo hawalitegemei sababu ni muda mfupi hukauka nakulazimika kuyafuata maji umbali wa kilomita 20  na shughuli zote za kujitafutia kipato husimama.

“Maji ya bwawa hilo sasa hivi huwezi kuona linatumiwa na jamii sababu ya mvua zinanyesha madimbwi mengi yamejaa maji mvua ikiacha kunyesha  vitongoji vyote sita hutegemea kwenye bwawa la shule hiyo kwaajili  ya kunywa na matumizi mengine ambayo siyo safi na salama isitoshe jamii nayo imekuwa ikijisaidia hovyo kwa kukosa  vyoo  ambavyo vimetitia kwa sababu ya mvua.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Buzali Mabele anasema kuwa  kweli kuna shida ya maji  kwenye kijiji hicho kilicho na vitongoji sita ambavyo ni mwamatembe,Mwasegagi,Mwakajala,Igunagahabi,Mwanjige na Mwamajigi nakutegemea bwawa la shule walililichimba hivi sasa huwezi kuona kama wanalihitaji sababu wanachota kwenye madimbwi mengine yaliyo na maji msimu huu wa mvua.
“Lakini  yakikauka  maji ya kwenye madimbwi  hulazimika kuchota  maji ya bwawa la shule  pia ukosefu wa vyoo katika kaya kujisaidia vichakani naona ni muda huu wa mvua kwani walikuwa na vyoo ingawa vilikuwa havina ubora vimetitia sababu ya mvua kubwa kunyesha na ardhi ilivyo ya kijijini hapo”anasema  Mabele.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Emanuel  Magesa anasema kuwa shule hiyo ilianzishwa mwaka 1981 na mpaka sasa ina jumla ya wanafunzi 480  wa darasa la awali  pekee ni 90  na  darasa la  kwanza ni 112 ambao ni wengi na umri wao  ni mdogo bado hawajafahamu matumizi ya matundu ya vyoo hata katika mazingira wanayotokea ndani ya familia zao hilo limekuwa changamoto  hali iliyopo wamekuwa wakijisaidia nje ya matundu ya vyoo  na katika mazingira ya shule ikiwa kuna bwawa la maji ambapo wamekuwa wakielimishwa.
Mtendaji  wa kijiji hicho  Thomas  Nyonyo anasema kuwa   bwawa la shule lilichimbwa kwa nguvu za wananchi baada ya kupata mradi wa lishe shuleni uliotolewa na shirika  la lishe  mwaka 2015 ambapo wanafunzi walihitajika kupata chakula kilichokuwa kikipikwa shuleni hapo na kuwepo uhaba mkubwa wa maji.
Nyonyo anasema  bwawa hilo limeweza kuwasaidia  wanafunzi kupata maji ya kunywa na jamii  ingawa kwa muda mfupi kwani  wanalazimika kuyafuata maji umbali wa kilomita 20 halmashauri ya wilaya ya Shinyanga  kata ya Iselamagazi  kijiji cha Ng’wang’osha.
Pia anasema wakitaka kufuata maji katika kijiji cha Bunambiyu kuliko na bomba la maji safi na salama  ni umbali  wa kilomita 15 kuyapata hivyo  kwa wastani kijiji chote hakina maji zaidi yakutegemea  bwawa lililopo shuleni ambapo maji yake nayo yanaonekana siyo safi na salama kutokana na mazingira yake.
“Bwawa hilo lililopo shuleni linahitaji utunzwaji na usimamizi mzuri ili kuepuka mlipuko wa magonjwa  katika jamii kwani hata upande wa jamii yenyewe umekuwa hauna vyoo bora  hivi sasa kipindi cha mvua  karibu vyoo vingi  kwenye kaya vimetitia nakufanya kujisaidia vichakani hovyo kikiwepo cha shule chenye matundu mawili nacho kimetitia pia”anasema  mtendaji wa kijiji Nyonyo.
Anasema mpango uliopo  ili kuweza kupata  maji safi na salama  ya kunywa  waliitisha kikao cha kijiji nakufikia maazimio ya kila kaya kuchangia kiasi cha shilingi 50,000 ili kuyavuta bomba la  maji kutoka kijiji cha Bunambiyu  nakuweza kupata maji safi na salama  na wananchi wamedai wako tayari wakati watakapo uza mazao yao ikiwa kijiji  hicho kina kaya 218 na idadi ya watu 1882.
Diwani wa kata ya Bunambiyu Richard Sangisangi anasema kuwa  kijiji hicho kweli hakina bomba kina shida ya maji  nani umbali mrefu kuyafuata maji kwani hata haya yaliyopo hayatoshelezi kwa idadi ya watu waliopo  kwenye kata nzima  hata miundombinu ya bomba hilo sio imara  limekuwa likihalibika  mara kwa mara.
Mganga msaidizi wa kituo cha afya Bunambiyu   Simba Rajabu anasema kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa kituoni hapo huja na magonjwa ya kuhara  idadi kubwa ni watoto  sababu ni kutokana na mazingira wanayoishi  nakutumia maji yasiyo safi na salama .
Dkt Rajabu anasema kuwa mara kwa mara wamekuwa wakiwapatia elimu juu ya afya zao na mazingira wanayoishi ya ukosefu wa matundu ya vyoo au kuwa na vyoo bora  kwani upande wa  huduma za maji ni shida kwao hupata maji yasiyo safi na salama  katika vyanzo vya maji na hawana desturi ya kuyachemsha ili kuua wadudu matokeo yake  kupatwa na magonjwa ya mlipuko kama kuhara walio wengi.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Stephen Magoiga  anasema kuwa kijiji hicho siyo pekee kuwa na changamoto ya  kukosa maji ni vijiji vingi hilo  linaeleweka  ila mpango uliopo  mradi wa  maji ya ziwa Victoria umeanza kuenea maeneo mengi jitihada zitafanyika kuvuta mabomba ili kuwarahisishia wananchi huduma yakupata maji karibu kwa mujibu wa sera ya maji  nakuondokana na kutafuta maji umbali mrefu.
Anasema  lipo suala la  jamii kukosa vyoo vyenye ubora  na msimu wa mvua kweli vimetitia  na matokeo yake baadhi  yao kuendelea kujisaidia vichakani  bila ya kujenga wanaweza kueta athari kwenye vyanzo vyao vya maji   lakini bado wanaendelea kila siku kuwapatia elimu juu ya utunzaji mazingira nakujenga vyoo vyenye ubora  ili kuepuka mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu na kuhara.
Halmashauri ya wilaya ya Kishapu ni miongoni mwa maeneo hapa nchini ni  kame  yasiyopata mvua za kutosha  ambapo asilimia 88 ya wakazi wake ni wafugaji na wakulima na  asilimia 27 ni wakulima pekee.
Hata hivyo Sera ya maji ya mwaka  2002 inaeleza kuwa uvunaji wa maji ya mvua  ni njia  muhimu yakupata  maji hususani katika maeneo kame ambako yanaweza kuwa ndio chanzo pekee cha maji  cha kuaminika  katika kipindi cha msimu wa kiangazi.
Pia moja ya uvunaji ya maji  wananchi  wanaoishi vijijini watahamasishwa  kutumia teknolojia  hii ikiwa ukosefu  wa maji safi na salama  na kutofuata  kanuni bora za afya  na usafi wa mazingira  ni  chanzo kikubwa  cha mlipuko wa magonjwa  na vifo  na husababisha wimbi la umasikini  hasa kwa wanawake na watoto.
Hata hivyo sera hiyo inaeleza kuwa ili kuboresha  afya ya jamii mkazo utawekwa  kwenye mipango ya pamoja  inayojumuisha  utoaji wa huduma  za maji,usafi wa mazingira  na elimu ya afya .

No comments:

Post a Comment