Mtandao huu bado upo kwenye matengenezo, punde utapata matukio katika picha, habari, makala na taarifa mbali za kijamii...Endelea kutufuatilia

Monday, May 28, 2018

Ukosefu wa maji na pedi shuleni unavyo mfedhehesha msichana awapo shuleni



Na Grace Mwakalinga, Mbeya
 “Kutokana na ukata wa fedha kutoka kwa wazazi wakati mwingine ninalazimika kutumia vitambaa ili kujisitiri, kwa siku ninatumia vitambaa vitatu mpaka vinne kulingana na hedhi inavyotoka, wakati wa mapumziko au nikiona nimezidiwa naenda chooni kubadilisha kitambaa kingine, sijisafishi ninavaa hivyovyo kwa sababu ya tatizo la maji hapa shuleni.” alisema Nchambi Petro, ambaye ni Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Imezu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Mkoani Mbeya, katika mahojiano na mwandishi wa Makala hii.
Petro ni Dada Mkuu wa Shule,  ambaye naye anaishi hosteli anadai ukosefu wa huduma ya maji  kunaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya masomo yao kwani  hutumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji kwenye mifereji na mito ambaye iko mbali na mazingira ya shule.
Petro anasema njia pekee ya kutatua changamoto hiyo ni  Serikali au wazazi kukubali kuweka matanki ya kuvuna na kuhifadhi maji katika shule yao wakati wa Mvua.
Wanafunzi  wa kike katika Shule ya Sekondari Imezu,  iliyopo katika Kata ya Inyala  Wilaya Mbeya, wengi wao wanatoka katika familia za kawaida  ambazo pia kipato cha wazazi ni kidogo.  Wengi wanashindwa kujisitiri na kufanya usafi wa maumbile yao kutokana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama shuleni hapo.
Wanafunzi hao wanadai kukosekana huduma ya maji kunachangia kwa kiasi kikubwa watoto wa kike  wanapokuwa kwenye hedhi kutoa harufu mbaya  kutokana na kukosa maji ya kujisafisha.
wasichana wa shule za Sekondari wakionesha Pedi ambazo wamepatiwa kama msaada kuwawezesha kuhudhuria masomo vizuri.
Wanasema wakati mwingine wakiwa shuleni hulazimika kuficha kiasi kidogo cha  maji ambayo wamechota  mtoni kwa ajili kujisafishia ili kukwepa fedheha mbele za wanafunzi wa kiume.
Tangu kuanza kwa kidato cha kwanza mwaka 2007, Shule hiyo haijawahi kupata huduma ya maji safi na salama licha ya kuwa na miundombinu ya mabomba ambayo hayatoi maji, hali inayowalazimu wanafunzi kuvunja vipindi vya masomo kufuata huduma ya maji kwenye mito na mifereji.
Licha ya  Shule ya Sekondari Imezu kujenga  mabweni kwa ajili ya watoto wa kike kwa lengo la  kuondoa changamoto za mimba kwa wanafunzi wanaotoka mbali, visa vya ubakaji na kuongeza ufaulu, lakini muitikio wa wazazi au walezi kupeleka hosteli watoto wao umekuwa mdogo kutokana na  changamoto ya maji.
Madhira ya maji shuleni hapo pia yametajwa na wanafunzi kuongeza utoro kwani wakati mwingine hulazimika kuondoka shuleni kutafuta maji ya kunywa matokeo yake  wanafunzi  kutorudi tena kwenye vipindi vingine vya masomo.
Sharon Msalilwa ni mwanafunzi wa kidato cha Tatu katika Shule hiyo ambaye anaishi hosteli anasema  changamoto ya maji imekuwa moja ya kikwazo kwa mtoto wa kike katika kupata elimu kwani awapo kwenye hedhi hukosa amani na morali ya kusoma.
Anasema wakati wa kipindi cha hedhi anashindwa kuzingatia masomo kwani muda wote anajihisi kuwa amechafuka au kuhadhirika mbele ya darasa licha ya kuwa amejisitiri.
Msalilwa anaongeza kuwa kukosekana kwa chumba maalum cha kubadilishia taulo za kike ni changamoto nyingine kwani hutumia vyoo vya kawaida ambavyo alieleza kuwa havina maji  na ni vichafu.
Anasema kukosekana kwa maji katika vyoo kunaweza kusababisha magonjwa ya U.T.I, kuhara na hata kipindupindu.
Ruth Mzinga  ni mwalimu na  mlezi wa wasichana katika shule ya sekondari Imezu, anasema ukosefu wa maji shuleni hapo unawaathiri kwa kiasi kikubwa wanafunzi  wa kike kutokana na kuwa maumbile yao kuhitaji zaidi matumizi ya maji.
Mwalimu Mzinga anasema  ukosefu wa maji shuleni hapo pia umechangia kwa kiasi kikubwa wazazi au walezi kutowapeleka mabinti wao hosteli.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Tibus Makona  amekiri kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa maji na kueleza kuwa anayeathirika zaidi na kadhia hiyo ni binti.
Anasema Shule haina uwezo wa kuleta maji licha ya kuwa kuna miundo mbinu ya mabomba ambayo alisema yanatoa maji mara moja kwa mwezi au wakati mwingine kutotoka kabisa.
Inasema idadi kubwa ya wanafunzi shuleni hapo ambayo kwa sasa  imefikia wanafunzi 862 wasichana wakiwa ni 488 na wavulana 374 inatoa taswira ya uhitaji mkubwa wa maji.
Makona  ameleeza kuwa katika kumsaidia mtoto wakati wa hedhi Shule imeweka utaratibu wa kununua dazani moja ya taulo za kike kwa kila mwezi kwa kutumia fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya kununulia madawa.
Amesema taulo hizo za kike hazikidhi mahitaji kwa wanafunzi wote wenye uhitaji lakini wanamsiadia binti ambaye amepata dharula awapo shuleni.
Hata hivyo Makona amesema kuwa hosteli inauwezo wa kubeba wanafunzi 160 lakini kwa sasa ina wanafunzi 34.
Akizungumzia kadhia ya maji Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Inyala, Mwalingo Kisemba,  alisema kuwa Serikali inatambua jinsi changamoto ya maji inavyoathiri elimu ya mtoto wa kike ambapo amesema kwa  sasa wamenunua tanki ambalo litatumika kuvunia na kuhifadhia maji katika kipindi hiki cha masika.
Licha ya kuwa Serikali imetoa msaada wa  tanki la Maji shuleni hapo ambalo bado halijatengenezwa miundo mbinu kwa ajili ya kutumika watahakikisha wanafanya haraka ili kunusuru hali hiyo.
“Mtoto wa kike hushindwa kuhudhuria masomo siku tano kila mwezi kutokana na sula la hedhi na miezi miwili kila mwaka, hali hii sio nzuri kwani utoro huo usababishwa na changamoto ya kukosa taulo za kujisitiri na ukosefu wa maji pia jitihada zinahitaji ili kuwasaidia mabinti zetu hawa,” alisema Mwalingo.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Mbeya, Zena Kapama alisema kuwa kwa kutambua changamoto wanazozipata watoto wa kike wawapo shuleni Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imetenga jumla ya shilingi milioni 1.6 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ununuzi wa tatulo za kike ambapo utekelezaji wake utazinufaisha shule za Sekondari 28 za Wilaya hiyo.
Kapama anasema wanatambua ukubwa wa tatizo kwa mabinti lakini kwa kuanzia itasaidia na kuahidi kuongeza bajeti wakati mwingine kadri fedha zitakapopatikana.
TGNP Mtandao ni taasisi inayojenga uwezo kwa wananchi kuibua suala la upatikanaji wa pedi za bure kwenye mikutano ya vijiji na mitaa na kuomba serikali za vijiji na kamati za maendeleo za Kata (WDC) kupanga kwenye bajeti zake ili shule za kata zitoe bure pedi kwa wasichana.
Hadi sasa halmashauri tatu ambazo watumishi wake wamejengewa uwezo na TGNP Mtandao zimeshapanga  fedha kwenye bajeti zake kuwezesha wasichana kupata bure pedi mashuleni. Halmashauri hizo ni Kishapu, Kisarawe na Mbeya.

No comments:

Post a Comment