SERA ya afya ya mwaka 2007 imeelekeza kuwa kila
kata inatakikwa kuwa na kituo cha afya na kila kijiji kuwa na Zahanati ili
kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi hasa wanaoishi maeneo ya
pembezoni.
Mkakati wa kufikia lengo la sera hiyo ni
Serikali kushirikiana na wananchi pamoja na wadau wengine ambapo pia serikali
inatakiwa kuhakikisha kunakuwepo na watoa huduma wa kutosha, vifaa tiba na dawa
katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Pia sera hiyo imesisitiza namna Serikali itakaposhirikiana na wadau na
wananchi katika juhudi za kupanua na kukarabati majengo ya kutolea huduma za
afya pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na uwiano wa kijiografia katika kutoa huduma za
afya nchini.
Utekelezwaji wa sera hiyo katika maeneo mengi
hasa ya pembezoni mwa miji bado haujafanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na
kuwepo kwa changamoto lukuki za upatikanaji wa huduma za afya.
Miongoni mwa sehemu ambazo hazijaguswa na Tamko
la Sera hiyo ni kata ya Itewe iliyopo katika halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,
ambayo ilianzishwa mwaka 2009, kutoka kwenye kata mama ya Iyela.
Kata ya Itewe ni Miongoni mwa kata 28 za
halmashauri ya Mbeya vijijini ikiwa ina
jumla ya watu 4655, kaya 1108 na ina jumla ya vijiji vitano ambavyo ni
Iyela-Nyara, Idunda, Tembela, Itewe na Isongwa.
Licha ya kata hiyo kuhudumia vijiji vitano
lakini hadi sasa haina kituo cha afya na wananchi wake wanategemea kupata
huduma katika zahanati moja tu ambayo ipo katika kijiji cha Idunda jambo ambalo
linaathiri kuzorota kwa huduma ya afya katika kata hiyo.
Hata hivyo zahanati hiyo haina Miundombinu
ambayo inakidhi mahitaji ya wagonjwa hasa akina mama wajawazito kwani ina
vitanda viwili tu, ambapo kati yake kimoja kinatumika kwa ajili ya kujifungulia
na kingine kwa ajili ya kupumzika.
Wanananchi hasa wanawake wanaoishi katika kata
hiyo wanapaza sauti zao kwa kuiomba serikali kuwajengea kituo cha afya au
kuboresha miundombinu ya zahanati hiyo ili waondokane na adha ya kutopata
huduma bora za afya.
Wanawake hao walitumia mbinu ya igizo kufikisha
kilio chao Mbele ya viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ili waione
changamoto yao, waichambue na kuifanyia utekelezaji kwa lengo la kuboresha
huduma za afya katika kata yao hasa kwa mama na mtoto.
Kupitia igizo hilo walionesha namna akina mama
wajawazito wanavyokuwa wanajifungulia njiani kutokana na kutembea umbali mrefu
kufuata huduma ya afya hadi katika zahanati ya kijiji cha Idunda ambayo
inahudumia kata nzima kutokana na kukosekana kwa kituo cha afya.
Pili Daniel, mkazi wa Itewe yeye aliigiza kama
mama mjamzito akionesha uhalisia wa mazingira yao ambapo alionesha namna wanawake
wajawazito wanavyojifungua njiani na wakati mwingine wanavyotozwa faini ya
10,000 na wahudumu wa afya kwa kosa la kujifungua njiani ama nyumbani.
Kupitia igizo hilo anasema umbali mrefu umekuwa
ukisabaisha wanawake wa kata hiyo kujifungulia nyumbani au njiani au wakifika
kwenye zahanati wanakosa sehemu ya kupumzikia kutokana na kukosekana kwa
kitanda.
“Huko zahanati hata maji hakuna, tunatumia ya
mtoni, wakati mwingine nesi anaenda kuchota au sisi wenyewe tunaenda mtoni
kuchota ili yatusaidie wakati wa kujifungua,” alisema
Igizo hilo limebeba uhalisia wa maisha
wanayopitia wananchi wa kata hiyo hasa wanawake, ambapo mkazi wa kata hiyo Wilbroa
Ndezi ameongezea kwa kusema kuwa wakati mwingine wamekuwa wakikosa dawa
wanapokuwa wamefika kwenye zahanati hiyo kwa ajili ya kupata matibabu jambo
ambalo linapelekea waende kununua kwenye maduka ya watu binafsi kwa gharama
kubwa.
Amesema licha ya kukata bima ya afya kupitia
mfuko wa bima ya afya ya Taifa (CHF) kwa gharama ya sh.12,000 kwa mwaka au
sh.6000 kwa mtu mmoja bado wamekuwa
wakikosa baadhi ya dawa.
“Kuna wakati unaona ni heri usiende zahanati,
kule unaweza kufika ukaelezwa kuwa dawa hamna nenda kanunue kwenye duka la
madawa la watu binafsi wakati wale wanaokuja kuandikisha bima walitueleza kila
kitu tutakipata pale zahanati,” alisema.
Edda Mwalima amesema kuna wakati mama mjamzito
akifika katika zahanati hiyo au Mgonjwa wa kawaida anakaa muda mrefu kusubiri
huduma kutokana na uhaba wa watumishi na wakati mwingine anarudu nyumbani bila
kupata huduma.
Amesema kukosekana kwa vitanda vya kupumzika
kumekuwa kukisababisha baadhi ya wanawake wajawazito kutoona umuhimu wa kwenda
zahanati na kuamua kujifungulia nyumbani jambo ambalo si salama kwa afya zao na
watoto wao.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa kata hiyo Michael mwaifweya
anakiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa wameanza kujenga miundombinu
Majengo kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa utoaji huduma katika zahanati hiyo.
Amesema majengo hayo yanajengwa kwa nguvu za
wananchi na kwamba yakikamilika yataondoa kero zilizopo na kuwa sasa wanatafuta
eneo ambalo litajengwa kituo cha afya cha kata.
Mganga mkuu wa Zahanati hiyo, Angel Mabula
amesema zahanati hiyo inawahudumu watatu na kwamba wanakidhi mahitaji ya
wagonjwa kwa kuwa idadi ya wagonjwa wanaofika kupata huduma ya afya kwa siku ni
wachache.
Amesema kwa siku wanawahudumia wagonjwa kwa
wastani wa watu 5 hadi 3 na wakati mwingine 10 hadi 15 kulingana na majira ya hali ya hewa ambapo
kwa wastani wa mwezi mmoja wajawazito 10 wanafika kliniki kwa ajili ya
kufuatilia maendeleo ya mtoto.
“Kwa siku anaweza kuja mjamzito mmoja hadi sita, lakini kwa watani wajawazito 100
wanafika kwa mwaka kuhudhuria kliniki, hapa kwenye zahanati kwa kweli hakuna
msongamano wa wagonjwa licha ya kuwa kata ina zahanati moja, kwa sababu
tumeweza kutoa elimu ya namna ya kuepukana na magonjwa yanayoweza kuzuilika na
wagonjwa wengine wanaenda kituo cha afya Inyala,” amesema
Amesema kwenye chumba cha kujifungulia (Labour
room) kuna vitanda viwili ambapo kimoja kinatumika kwa ajili ya kujifungulia na
kingine kwa ajili ya kupumzika hivyo inapotokea wamepokea wagonjwa wengi
inakuwa ni vigumu kuwamudu hivyo wengine wanalazimika kupumzika kwenye kitanda
cha wagonjwa wa kawaida ambacho kipo kimoja.
Amesema kwa kuwa vijiji vingi vipo mbali na
zahanati wakati mwingine wanalazimika kufanya kazi nje ya kituo kwa kuwafuata
wananchi na kutoa huduma za kuwapima watoto na wanawake wajawazito na kwamba
wameagiza kila kijiji kinunue kitanda na godoro kwa ajili ya kupumzikia
wagonjwa.
Amebainisha kuwa kwa takwimu za mwaka 2017
wajawazito 48 walijifungulia kituoni hapo wakati tisa wakijifungulia njiani ama
nyumbani ambapo kwa mwaka huo kiliripotiwa kifo cha mwanamke mmoja ambaye
alijifungulia nyumbani.
“ Mwaka jana watoto sita chini ya umri wa mwezi
mmoja walifariki dunia katika jamii hii,chini ya mwaka mmoja kifo kilikuwa
kimoja na chini ya miaka mitano vifo vilikuwa n inane,” alisema
Amesema dawa zote muhimu zipo za kutosha katika
zahanati hiyo na wakati mwingine zinapita muda wake wa matumizi (expire date)
kutokana na idadi ndogo ya wagonjwa wanaofika katka zahanati hiyo.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo
Zena Kapama amesema serikali inatatua changamoto za wananchi kutokana na
kipaumbele chao walichokiibua kupitia mikutano yao na kamati ya maendeleo ya
kata (WDC) na kuwasilishwa kwenye halmashauri.
Amesema kwa sasa wananchi wanapaswa kuibua
mradi kulingana na huduma wanayohitaji na kuanza kuitekeleza na serikal jukumu
lake ni kumalizia na kuleta watumishi kwa ajili ya kutoa huduma na kwamba suala
la afya si kipaumbele kwa sasa kwani halijaletwa katika bajeti ya mwaka wa
fedha 2018/19.
Hata hivyo serikali mkoani Mbeya imeanza
mikakati maalumu ya kuimarisha afya ya msingi kwa wananchi ili kuimarisha nguvu
kazi kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa Viwanda na shughuli za
kilimo.
Moja ya mikakati iliyoanzishwa na Serikali hiyo
ni Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, kuwafunga vitanzi wakuu wa Wilaya zote za
Mkoa huo kwa kuwasainisha Mkataba maalumu wa uhamasishaji wa ujenzi wa vituo
vya Afya kwenye kila Kata, ujenzi wa Zahanati kila kijiji na kuwahamasisha
wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Mkataba kama huo ulisainiwa kati ya Kaimu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Nyasebwa Chimagu na wakurugenzi watendaji wa
Halmashauri zote za Mkoa huo.
Akizungumza na wakuu wa Wilaya, wakurugenzi wa
Halmashauri zote, Waganga wakuu wa Wilaya na maofisa watendaji wa Kata zote za
Mkoa wa Mbeya , Makalla amesema mkataba huo unawasisitiza viongozi hao kwenda
kuwahamasisha wananchi kujenga maboma ya vituo vya Afya kwenye Kata zao na
Zahanati kwenye vijiji ili Serikali imalizie kwenye uezekaji.
Amesema Mkoa wa Mbeya una jumla ya Kata 178
lakini zenye vituo vya Afya ni 25 pekee, huku vijiji 300 kati ya 533 ndio
vikiwa havina zahanati kama inavyotakiwa.
“Hatuwezi tukawa tunasema Hapa kazi tu! Na
kusisitiza uchumi wa viwanda wakati wananchi wetu hawana uhakika wa kupata huduma
za afya jirani na maeneo yao, hivyo Mkataba huu utamlazimisha kila mtu
kuhakikisha tunaimarisha afya za watu wetu,” amesema Makalla.
Hata hivyo amesema ili kuweka msisitizo wa
Mkataba huo nakala zake atazituma kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na
Serikali za mitaa, Sulemani Jafo na Makatibu wakuu wa Wizara hizo.
Makala amesema watahakikisha wanahamasisha
wananchi kwa kuanzia na viongozi wao ili mpaka kufikia mwaka 2020 kila kijiji
kiwe tayari kina Zahanati, kila Kata iwe na Kituo cha Afya na asilimia 100 ya
wananchi wawe wamejiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Mwisho.
No comments:
Post a Comment